TUME ya Taifa
ya Uchaguzi (NEC), imeanza kusambaza vifaa vyenye thamani ya Sh bil 41.6 kwa
ajili ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25.Kaimu Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi wa
NEC, Eliudi Njaila aliwaeleza wanahabari Dar es Salaam kuwa vifaa hivyo
vilianza kusambazwa jana kuelekea katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Kaimu Mkurugenzi
wa Ununuzi na Ugavi wa NEC, Eliudi Njaila
akiwaonesha
waandishi wa habari (hawapo pichani)
vifaa vya uchaguzi
vilivyoanza kusambazwa
Kanda ya Ziwa, Dar
es Salaam jana.
|
Alivitaja kuwa ni pamoja na vibanda vya kupigia kura
(Vituturi) vitakavyotumiwa na walemavu kwa mara ya kwanza katika uchaguzi wa
mwaka huu.
Vifaa vingine muhimu vilivyotajwa ni masanduku ya
kupigia kura na lakini za kufungia masanduku hayo.
Kwa mujibu wa Njaila, vituturi 70,000 vitasambazwa
katika kila kituo, ambapo kulingana na maelezo ya mzabuni kwa tume hiyo,
atakabidhi vituturi 8,000 kwa halmashauri husika kila siku.
Njaila alisema, wataanza kusambaza vifaa hivyo katika
mikoa ya Kagera, Mara, Geita, Mwanza, Simiyu na Shinyanga na kufuatiwa na mikoa
ya kanda ya Tabora, Dodoma, Singida, Rukwa, Katavi na Kigoma. Alisema baada ya
hapo vifaa hivyo vitapelekwa Mtwara na Lindi, kisha kupelekwa Mbeya, Iringa,
Ruvuma na Njombe.
“Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na ya Kanda ya
Mashariki yaani Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Zanzibar na Pemba vitamalizwa
kusambazwa Oktoba 15”, alisema.
Aliongeza kuwa Septemba 29, mwaka huu wataanza kupokea
karatasi za kupigia kura kwa kanda kutoka nchini Afrika Kusini hivyo kumaliza
upokeaji wa vifaa vyote Oktoba 15.
Njaila alisema walemavu wasioona wana karatasi zao
maalum. Alisema vifaa vya kufungia maboksi ya kura vitakuwa vya aina mbili; vya
rangi nyekundu vitakavyotumika katika mafunzo kwa wasimamizi na vya bluu
vitakavyotumika wakati wa uchaguzi.
“Maboksi ya kupigia kura yatakuwa na mifuniko ya rangi
tofauti. Yenye mifuniko ya rangi nyeusi yatatumika kwa madiwani, nyekundu
wabunge na bluu kwa ajili ya kura za marais,” alisema.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri
Mkuu, Florens Turuka alisema serikali itaipa NEC fedha zinazohitajika itekeleze
majukumu yake ipasavyo.
No comments:
Post a Comment