JAMAL MALINZI |
RAIS MALINZI AELEZEA SIKU 100 ZA
UTEKELEZAJI WA ILANI
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ameelezea hatua zilizofikiwa katika utekelezaji
wa Ilani yake siku 100 tangu alipoingia madarakani.
Akizungumza na waandishi wa habari leo
(Februari 7 mwaka huu) katika mkutano uliofanyika katika hoteli ya Hyatt
Regency jijini Dar es Salaam, Rais Malinzi aliainisha maeneo kadhaa yaliyopewa
kipaumbele na tayari yameanza kufanyiwa kazi pamoja na changamoto zilizopo.
Alisema muundo wa Idara ya Ufundi
umebadilishwa kwa kuundwa vitengo vya ufundi, elimu na maendeleo ya mpira wa
miguu huku maeneo ambayo tayari yameanza kufanyiwa kazi kuwa ni;
Ujenzi wa kituo cha mpira wa miguu
(football centre of excellency), timu kupanda daraja, kuanzisha mashindano
mapya na kufufua ya zamani, mpira wa miguu wa wanawake, maandalizi ya vijana
(grassroot football), tiba, walimu na makocha, utawala, uhusiano na Zanzibar,
klabu za mpira wa miguu, wachezaji, masoko na uwekezaji, kitengo cha habari,
viwanja na timu ya Taifa (Taifa Stars).
Rais Malinzi amesema changamoto
zilizopo kwa sasa ni matumizi ya tiketi za elektroniki, ufinyu wa bajeti,
madeni, nidhamu, maadili na uchezeshaji wa waamuzi.
Ametoa mwito kwa wadau wote nchini
wakiongozwa na Serikali, Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA),
Afrika (CAF), Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), vyombo vya habari, mashirika
ya umma na kampuni binafsi kushikamana na kuwa kitu kimoja kwa nia ya kuinua
kiwango cha mpira wa miguu Tanzania. (TAARIFA NZIMA YA RAIS IMEAMBATANISHWA)
KILA LA KHERI YANGA, AZAM
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) linazitakia kila la kheri klabu za Yanga na Azam ambazo timu zake
zinatuwakilisha kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CL) na Kombe la
Shirikisho (CC).
Yanga inacheza na Komorozine ya Comoro
katika mechi ya kwanza ya raundi ya awali ya CL itakayochezwa kesho (Februari 8
mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
Nayo Azam inaikaribisha Ferroviario de
Beira ya Msumbiji katika mchezo wa kwanza wa raundi ya awali ya CC utakaochezwa
Jumapili (Februari 9 mwaka huu) saa 10 kamili kwenye Uwanja wa Azam Complex
uliopo Chamazi, Dar es Salaam.
Ni matumaini yetu kuwa timu hizo mbili
zitatuwakilisha vizuri kwenye michuano hiyo, na kuwataka Watanzania wajitokeze
kwa wingi viwanjani kuziunga mkono hasa kwa vile zinacheza nyumbani.
TWIGA STARS YAHAMISHIA KAMBI DAR
Timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya
wanawake (Twiga Stars) imehamishia kambi yake jijini Dar es Salaam kutoka Mlandizi
mkoani Pwani ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mechi ya michuano ya Afrika (AWC)
dhidi ya Zambia.
Kikosi hicho chini ya Kocha Rogasian
Kaijage kimepiga kambi katika hosteli ya Msimbazi Center kikiwa na wachezaji 25
kutoka 30 ambao kilianza nao katika kambi ya Mlandizi mkoani Pwani.
Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya
kwanza dhidi ya Zambia itachezwa Februari 14 kwenye Uwanja wa Nkoloma jijini
Lusaka. Timu zitarudiana wiki mbili baadaye jijini Dar es Salaam.
Wachezaji waliopo katika kikosi hicho
ni Amina Ally, Amisa Athuman, Anastasia Anthony, Asha Rashid, Esther Chabruma,
Eto Mlenzi, Evelyn Sekikubo, Fatuma Bashiri, Fatuma Hassan, Fatuma Issa, Fatuma
Mustafa na Fatuma Omari.
Wengine ni Flora Kayanda, Happiness
Hezron, Maimuna Said, Mwajuma Abdallah, Mwapewa Mtumwa, Najiat Abbas, Pulkeria
Charaji, Shelder Boniface, Sophia Mwasikili, Therese Yona, Vumilia Maarifa,
Winfrida Daniel na Zena Khamis.
PRISONS, RUVU SHOOTING KUUMANA SOKOINE
Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL)
kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho (Februari 8 mwaka huu) kwa
mechi moja kati ya Tanzania Prisons na Ruvu Shooting itakayofanyika Uwanja wa
Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Mechi nyingine nne za ligi hiyo
zitachezwa keshokutwa (Februari 9 mwaka huu) kwenye viwanja mbalimbali. Mgambo
Shooting vs Simba (Mkwakwani, Tanga), Oljoro JKT vs Kagera Sugar (Sheikh Kaluta
Amri Abeid, Arusha), Rhino Rangers vs Coastal Union (Ali Hassan Mwinyi, Tabora)
na Mbeya City vs Mtibwa Sugar (Sokoine, Mbeya).
FDL YAANZA VUMBI LA MZUNGUKO WA PILI
Mzunguko wa pili wa Ligi Daraja la
Kwanza (FDL) unaanza kesho (Februari 8 mwaka huu) kwa mechi za kundi A na B
wakati kundi C lenyewe litaanza mechi zake Februari 22 mwaka huu.
Mechi za kundi A ni Green Warriors vs
Tessema (Uwanja wa Mabatini, Mlandizi), Polisi Dar es Salaam vs Transit Camp
(Uwanja wa Karume, Dar es Salaam). Februari 9 mwaka huu ni African Lyon vs
Villa Squad (Uwanja wa Mabatini, Mlandizi) na Friends Rangers vs Ndanda (Uwanja
wa Karume, Dar es Salaam).
Kundi B kwa kesho (Februari 8 mwaka
huu) ni Polisi Morogoro vs Burkina Faso (Jamhuri, Morogoro), Lipuli vs Mkamba
Rangers (Samora, Iringa), Kurugenzi vs Kimondo (Wambi, Mufindi) na Mlale JKT vs
Majimaji (Majimaji, Songea).
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari na Mawasiliano
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF)
TANZANIA FOOTBALL
FEDERATION
TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA ILANI YA
UCHAGUZI
YA RAIS WA TFF
Ndugu zangu,
Uchaguzi mkuu wa TFF ulifanyika tarehe
27 Oktoba, 2013 na kukamilika alfajiri ya tarehe 28 Oktoba, 2013 ambapo Kamati
ya Utendaji ya TFF ilitangazwa rasmi na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya
Uchaguzi wa TFF Ndugu Hamidu Mbwezeleni.
Katika kuelekea uchaguzi mkuu huo
niliitisha mkutano na waandishi wa habari ambapo nilitangaza ilani yangu ya
uchaguzi. Lengo la ilani ilikuwa ni kuwaeleza wadau na wapenzi wa mpira
wa miguu Tanzania dira ambayo ingeongoza mpira wetu iwapo ningechaguliwa kuwa
Rais wa TFF. Aidha niliahidi iwapo ningechaguliwa tungekutana katika
chumba hiki hiki baada ya siku 100. Ninapenda nichukue fursa
hii kuwashukuru na kuwapongeza wajumbe wote wa Mkutano Mkuu wa TFF,
walionipa kura na ambao hawakunipa kura, kwa kukamilisha vyema zoezi la
uchaguzi huo. Uchaguzi umekamilika kazi iliyobakia mbele yetu ni
kutekeleza majukumu yetu kama viongozi wa mpira miguu Tanzania.
Ilani na Utekelezaji wake
Ilani yangu ya uchaguzi iliainisha
maeneo kadhaa ya kupewa vipaumbele. Nitakumbushia maeneo haya na kueleza
hatua tulizofikia katika utekelezaji wake:
1. 1. Idara ya Ufundi
1.1
Kikao cha Kamati ya Utendaji kilichokaa tarehe 23 Novemba, 2013 pamoja na mambo
mengine kilipitisha muundo mpya wa Sekretariati ya TFF.
1.1
Muundo huo unaelezwa katika chati hii hapa chini:
Katika muundo huu Idara ya
Ufundi imepanuliwa kwa kuundwa vitengo vya Ufundi,Elimu na Maendeleo ya mpira.
Aidha katika kutekeleza azma ya
kuboresha usimamizi wa mpira wa vijana (Youth Football) Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania limeamua kuajiri Desk Officer wa vijana yaani msimamizi maalum
wa mpira wa vijana na tayari ameajiriwa.
Zoezi la kuimarisha Idara ya Ufundi
kwa kuajiri Mkurugenzi wa Ufundi pamoja na Wakurugenzi wake Wasaidizi
linaendelea.
1.2
Ujenzi wa Kituo cha Mpira (Football Centre of Excellency)
Limekuwa ni jambo la kufurahisha na
kutia moyo kuwa mara baada ya kuingia madarakani Serikali kupitia Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ilitufahamisha juu ya uamuzi wa Serikali,
kwa kushirikiana na Kampuni ya SYMBION ya Marekani na Klabu ya Mpira ya
SUNDERLAND ya Uingereza, wa kujenga kituo cha michezo (Sports Centre) Kidongo
Chekundu , Ilala na kujenga kituo cha kulea na kukuza vipaji vya vijana (Elite
Academy) Wilayani Kinondoni. Wizara ilinikutanisha na Uongozi wa SYMBION
na mazungumzo yanaendela kuona ni jinsi gani mradi huu utashirikisha Serikali,
Mshirika wetu SYMBION, Klabu ya SUNDERLAND na TFF ambao kwa mujibu wa katiba
yetu ndio waratibu na wasimamizi wa maendeleo ya mpira wa miguu
Tanzania. Vikao kadhaa vimefanyika na mwelekeo ni mzuri sana.
Tunaamini mradi huu utatoa mchango mkubwa sana katika kuendeleza mpira wa
vijana (Youth Football).
Aidha kamati ya utendaji ya TFF
imeviagiza vyama vyote vya mpira vya mikoa kuomba kumilikishwa viwanja vikubwa
katika maeneo mapya yanayopimwa, TFF italipia malipo yote yatakayotakiwa.
Mkoa wa Tanga tayari wametekeleza agizo hili na hati imekwisha toka.Msanifu
tayari anaanda michoro ya awali kwa ajili ya kujenga kituo cha michezo katika
ardhi hii. Mfano wa mchoro wa kituo hiki ndio utakaotumika nchi nzima iwapo
utapitishwa na kamati ya utendaji.
1.3
Timu Kupanda Daraja
TFF tayari imeunda Kamati ya dharura
(Adhoc) ya kuangalia mapungufu yaliyopo katika utaratibu wa sasa wa kuwa na
timu 14 za Ligi Kuu na 24 za Ligi Daraja la Kwanza ili tuone ni kwa jinsi gani
tutaweza kuboresha Ligi yetu. Ripoti ya Kamati ikikamilika italetwa mbele
ya Kamati ya Utendaji kwa ajili ya maamuzi ya mwisho.
1.4
Kuanzisha Mashindano Mapya na Kufufua ya Zamani
Juhudi zinaendelea kuhakikisha
mashindano ya Kombe la Taifa yanafufuliwa. Aidha taratibu za kuanzisha
upya Kombe la Shirikisho (Federation Cup) ambalo litakuwa ni la mtoano nchi
nzima zimefikia hatua nzuri na muda si mrefu taratibu zake zitatangazwa
pindi mshirika wetu atakapokuwa amemaliza maandalizi upande wake.
1.5
Mpira wa Wanawake
1.5.1 Katika
kuhakikisha mpira wa wanawake unatengenezwa mkakati maalum wa maendeleo
matayarisho ya mpango wa maendeleo ya mpira wa wanawake (women football
development plan) yamekamilika na yatawasilishwa katika kikao kijacho cha
Kamati ya Utendaji kwa ajili ya maamuzi ya mwisho. Mpango huu utatoa dira
ya maendeleo ya mpira wa miguu kwa miaka mitano ijayo na utakuwa ni
sehemu ya mpango kazi wa TFF wa miaka mitano.
1.5.2 TFF inayo
furaha pia kuufahamisha umma wa wapenda mpira wa Tanzania kuwa shula ya kukuza
na kuendeleza vipaji ya Alliance Mwanza kwa kutambua mapungufu yaliyopo katika
kuendeleza mpira wa wanawake kuanzia mwaka huu imeanzisha mafunzo maalum ya
mpira wa watoto wa kike umri chini ya miaka 10. Matunda yake tutayaona
baadaye. Hawa watakuzwa na kulelewa pamoja.
1.5.3 Jitihada
zinafanyika kuanza mashindano ya kitaifa ya wanawake na muda si mrefu utaratibu
wake utatangazwa baada ya mshirika wetu kumaliza maandalizi yake.
1.5.4 TFF kwa
kushirikiana na Wizara ya Wanawake na Jinsia ipo katika kuandaa mpango
kazi wa kushirikiana na vyuo 55 vya Ustawi wa Jamii Tanzania katika kuanzisha
masomo maalum kwa wasichana katika vyuo nchini, masomo ambayo yatahusisha
ufundishaji wa mpira wa wanawake, urefa, ukocha na utawala wa mpira.
Lengo ni kutoa fursa kwa wasichana kujifunza stadi hizi kama sehemu ya masomo
yao katika vyuo vya maendeleo ya jamii. Utaratibu wa mpango huu
unasimamiwa na chama cha mpira wa migu wa wanawake (TWFA) na taasisi nyingine
husika.
1.5.5 Pamoja na
ufinyu wa bajeti tulionao na timu zetu za wanawake kutokuwa na udhamini TFF
bado inahakikisha timu zetu za wanawake zinashiriki michuano yote ya
kimataifa.Wiki iliyopita timu yetu ya Taifa ya wanawake imesajiliwa kushiriki
mtoano wa kushiriki fainali za All Africa games Congo Brazzavile 2015.
1.6
Maandalizi ya Vijana (Grassroot Football)
Mpango kazi wa maendeleo ya mpira wa
miguu wa vijana Tanzania (Tanzania youth development plan)
maandalizi yake yamekamilika na utazinduliwa muda si mrefu.
Vipaumbele vikuu vya mpango huu ni pamoja na:
1.6.1 Kuhakikisha
shule zote za msingi 16,000 za Tanzania zinakuwa na viwanja
vya kuchezea mpira, mwalimu mmoja wa mpira na zinapata kwa mwaka
angalau mipira 10 ya size 3 na 4 pamoja na jozi angalau 30 za viatu.
TFF tayari inawasiliana na Mashirika
mbalimbali yasiyo ya kiserikali ili yatukusanyie vifaa vya mpira vilivyotumika
(has viatu) ili viweze kuletwa na kugawiwa kwa watoto wetu kwenye shule za
msingi na academies. Kwa sasa tayari kontena mbili za vifaa hivi
zimekwisha kusanywa nchini Uingereza na utaratibu wa kuzileta
unafanyika. Lengo ni kuingiza nchini jozi za viatu 500,000 kwa mwaka na
mipira 160,000 ya size 3 na 4 kwa mwaka. TFF inaomba ushirikiano wa Serikalini,
Taasisi za Umma, Makampuni Binafsi na Taasisi zisizo za kiserikali katika
kuhitimisha azma hii.
1.6.2 TFF ilipata
fursa ya kukutana na Balozi wa Uholanzi hapa nchini na kufanya naye
mazungumzo. Nia na lengo ilikuwa ni kuangalia ni kwa jinsi gani Uholanzi
inaweza kutusaidia kufundisha walimu wa walimu (trainer of trainers).
Matumaini yetu ni kuwa walimu hawa wakishafuzu watakuwa na jukumu la
kuwafundisha walimu wa michezo wa shule za msingi kwa kushirikisha vyuo vya
walimu vinavyotoa taaluma hii kama Malya, Murutunguru na Butimba.
1.6.3 TFF kwa
kushirikiana na taasisi isiyo ya kiserikali inaangalia uwezekano wa kujenga
vituo vya michezo 169 katika Wilaya zote 169 Tanzania. Vituo hivi pamoja
na kufundisha mpira vitakuwa pia ni vituo maalum vya kuwafundisha vijana juu ya
athari za matumizi ya dawa za kulevya.
1.6.4 TFF kupitia
Idara yake ya Ufundi na Kamati ya Vijana iko mbioni kufanya sensa ya vituo vya
kukuza na kulea vipaji vya vijana (Academies) pamoja na vituo vya mpira (Sports
Centres) nchini kote Tanzania. Utaratibu unafanywa wa kuweka vigezo vya
kutambuliwa vituo hivi na TFF itaanzisha utaratibu wa kusajili na kutoa vyeti
vya usajili kwa vituo vitakavyokidhi vigezo. Lengo ni kuweka utaratibu
nchini wa kusimamia na kuendeleza vituo hivi kitaifa.
1.6.5 Mpango wa muda
mfupi wa TFF ni kuandaa timu ya Taifa ya vijana itakayoshiriki mashindano ya
Fainali za Afrika umri chini ya miaka 17 mwaka 2019. Tanzania tumeomba
uenyeji wa Fainali hizi. Mwaka huu wa 2014 TFF itafanya mashindano maalum
ya vijana chini ya umri wa miaka 12 ili kuunda timu ya Taifa ya kuanzia ya U12,
timu ambayo itakua pamoja kuelekea 2019. Malengo ni kuiboresha timu hii
kila mwaka kwa kuongeza vijana U13 mwaka 2015, U14 mwaka 2016, U15 mwaka 2017
na mwishowe U16 mwaka 2018.TFF imekwisha pata mshirika wa mpango huu na
akimaliza maandalizi yake atatangazwa rasmi.
1.6.6 Ili Tanzania
ifundishe mpira unaofanana nchini kote, utaratibu unafanyika wa kuandaa mtaala
wa kufundisha mpira (National football curricullum). Mtaala huu
unaandaliwa na Idara ya Ufundi ya TFF kwa kusaidiana na Mtaalam wa mpira toka
Uholanzi. Mtaala huu ukikamilika utakuwa nyenzo muhimu ya kufundishia
mpira mashuleni na kwenye Academies.
1.7
Tiba, Waalimu na Makocha
TFF imeandaa mpango wa kukutana na
wenyeviti wa vyama vya Tiba, Waamuzi na Makocha ili kupanga nao mikakati ya
maendeleo ya kitaaluma. Mikakati hii ikiwa tayari itajumuishwa katika
mpango mama wa maendeleo wa TFF (TFF National Business Plan), mpango
ambao maandalizi yake yatakamilika ndani ya miezi mitatu kuanzia sasa.
1.8 Utawala
TFF imeanza kwa kuboresha mazingara ya
utendaji wa kazi. Vyama shiriki TAFCA, FRAT, TASMA, TWFA na SPUTANZA
tayari vimepatiwa ofisi za kisasa katika eneo la Ilala. Ofisi kuu za TFF
nazo ziko mbioni kuhamia katika jengo la kisasa la PPF Tower,nia ikiwa ni
kuiwekea sekretariet ya TFF mazingira ya kisasa ya kufanyia kazi na pia kupisha
ujenzi wa kitega uchumi eneo letu la Uwanja wa Karume.
Aidha TFF imeunda kamati maalum
(Adhoc) ya kupitia Muundo wa Bodi ya Ligi lengo likiwa ni kutekeleza maagizo ya
Mkutano Mkuu wa TFF ulioagiza Bodi ya Ligi iundwe ikiwa ni ya mpito kuelekea
uundwaji wa Kampuni ya kuendesha Ligi Kuu ya mpira wa miguu.
1.9 Mahusiano
na Zanzibar
Mahusiano kati ya TFF na Chama cha
mpira Zanzibar (ZFA) yamezidi kuimarishwa kufuatia ziara kadhaa ambazo
tumezifanya kati ya maeneo yetu mawili. Mipango ya kuimarisha timu zetu
za Taifa za wakubwa, za vijana na za wanawake inafanywa kwa pamoja.
Juhudi za kuhakikisha Zanzibar inajiunga na FIFA pia zinaendelea kupitia
mazungumzo na wahusika.
1.10 Vilabu vya Mpira
Mara baada ya kuingia madarakani
Uongozi wa TFF ulikutana na viongozi wa vilabu vyote vya Ligi Kuu na Ligi
Daraja la Kwanza. Kikao hiki kilifanyika kama sehemu ya kuangalia ni
maboresho gani yafanyike ili kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa Ligi
zetu. Utekelezaji wa maazimio ya kikao hicho unaendelea kupitia wahusika
mbalimbali.
1.11 Wachezaji
SPUTANZA wameleta TFF mapendekezo yao
ya jinsi ya kuboresha maslahi ya wachezaji wa mpira wawapo mpirani na baada ya
kustaafu kucheza soka. TFF inayafanyia kazi mapendekezo hayo.
Lakini kubwa litakuwa ni kuanzisha Mfuko Maalum (Trust Fund) utakaochangiwa na
wachezaji wakiwa bado wanacheza pamoja na TFF na taasisi nyingine ili mfuko huu
uwasaidie pindi wakistaafu.
1.12 Masoko na
Uwekezaji
Kama nilivyoeleza hapo juu TFF iko
mbioni kuwekeza katika Kiwanja cha Karume, lakni pia njia nyingine za
kuiongezea TFF mapato ziko mbioni kuanzishwa ikiwa ni pamoja na kuanzisha
utaratibu maalum wa kuuza jezi za Timu ya Taifa (replica shirts).
1.13 Kitengo cha Habari
TFF imeandaa utaratibu wa kuboresha
kitengo hiki kwa kukiongezea nguvu kazi ili upashanaji wa habari uwe ni wa
haraka zaidi ikiwa ni pamoja na TFF kuanzisha Blog yake,kuboresha Tovuti
yake, na kuwa na kurasa kwenye mitandao ya kijamii kama Instagram, Facebook,
Twitter, n.k. Press officer ataajiriwa punde ili kuimarisha kitengo hiki.
1.14 Viwanja
Wakati tunaingia madarakani FIFA
kupitia mpango wake wa maendeleo ilikuwa imekwisha tenga pesa kwa ajili
ya kuweza nyasi bandia uwanja wa kihistora wa Nyamagana jijini
Mwanza. Uongozi wetu kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Meya wa Manispaa
ya Mwanza tulifuatilia kwa karibu na kufanikiwa kuondoa dosari zilizokuwa
zimekwamisha mradi huu. Utandazaji wa nyasi bandia utaanza mara moja
kuanzia sasa.
Kwa mafanikio haya Tanzania tuna
viwanja vyenye/ vitakavyokuwa na nyasi bandia baadae ambavyo ni Gombani Pemba,
Amani Zanzibar,Uwanja wa Uhuru, Uwanja wa Karume, Uwanja wa Azam Chamazi na
Uwanja wa Nyamagana.
TFF iko mbioni kuanza mazungumzo na
baadhi ya vyama vya siasa ambavyo ni wamiliki wa viwanja kadhaa vya mpira ili
kuangalia uwezekano wa kuingia ubia kwa nia ya kuviendeleza.
1.15 Timu ya Taifa
(Taifa Stars)
Ili kuandaa mkakati maalum wa
kuboresha timu ya Taifa TFF iliitisha kikao maalum cha walimu wa mpira
waandamizi. Kikao hiki kilifanyika Zanzibar kati ya tarehe 06-07 Desemba,
2013 na kilitoka na maamuzi kadhaa. Tarehe 18-19 Januari, 2014 TFF
iliitisha kikao kingine maalum cha Makatibu 30 wa vyama vya mpira vya mikoa
yote ya Tanzania Bara na Zanzibar ajenda ikiwa ni uboreshaji wa Timu ya Taifa
(Taifa Stars). Matunda ya vikao hivi ni mpango kazi maalum ulioandaliwa
wa kuboresha timu ya Taifa kwa kushirikiana na washirika wetu Tanzania
Breweries ltd kupitia bia yao ya Kilimanjaro Lager. Mpango huu utatangazwa
rasmi wiki ya pili ya mwezi February 2014.
CHANGAMOTO:
Uongozi mpya tangia umeingia
madarakani umekutana na changamoto kadhaa. Baadhi yake ni kama hizi zifuatazo:
1.Tiketi za Elektronik.
Uongozi mpya ulipoingia madarakani
ulikuta awamu iliyopita ilikwisha saini mkataba wa mradi huu.Jukumu la uongozi
wangu ni kutekeleza masharti ya mkataba. Changamoto nyingi zimejitokeza ikiwa
ni pamoja na mitambo kuzima mara kwa mara,mitambo kufanya kazi kwa spidi ndogo
, mageti yaliyofungwa mashine hizi kuwa machache (mfano Mkwakwani yamefungwa
mitambo miwili katika uwanja unaoingiza watu zaidi ya elfu kumi,uwanja wa Taifa
mitambo 48 wakati unaingiza watu 60,000,linganisha na uwanja wa Emirates London
unaoingiza watu 60,000 mitambo imefungwa 125,karibia mara tatu ya uwanja wetu
wa Taifa).
Pia uelewa mdogo wa wadau kuhusu taratibu za utumiaji tiketi hizi
nao ni tatizo na mkataba wa TFF na CRDB unaitaka TFF ibebe jukumu la kutoa
elimu kwa umma kuhusu matumizi ya tiketi hizi na bajeti yake haipungui
shilingi milioni 500 ikijumuisha gharama za matangazo kwenye
radio,magazeti,televisheni,roadshows,mabango,vipeperushi n.k. Matokeo yake
yalikuwa ni vurugu katika baadhi ya viwanja, vurugu ambazo kama si busara za
TFF zingeweza kusababisha maafa.
Mazungumzo yanaendelea kati ya TFF na mzabuni
CRDB ili kutafuta namna ya kuboresha utaratibu wa mfumo wa tiketi za
elektronik,lakini pia ni kuangalia ni kwa jinsi gani tiketi hizi hazigeuki kuwa
mzigo kwa mlaji maana licha ya watazamaji kulipia gharama ya tiketi yenyewe
lakini bado kuna asilimia inakatwa kama kamisheni ya uwakala jambo ambalo pia
ni mzigo kwa vilabu.TFF ina nia thabiti ya kutumia utaratibu huu,ni mzuri iwapo
utatekelezwa kwa taratibu stahili.
1. 2. Ufinyu wa bajeti
TFF katika kutimiza majukumu yake
inahitaji pesa nyingi hasa kuendeleza mpira wa vijana, kukidhi gharama za
kuendesha ofisi, kuvipa nguvu vyama wanachama na kusimamia timu zake nane za
Taifa (Za wakubwa mbili wanawake/wanaume,U17 mbili,U20 mbili na za olimpiki
mbili).Eneo lenye ufadhili mkubwa ni timu ya Taifa ya wanaume tu.Hivyo ni
dhahiri mahitaji ya fedha TFF ni makubwa sana na vyanzo havikidhi.Jitihada zinafanyika
kuhakikisha tunaongeza vyanzo mbadala wa mapato.
1. 3. Madeni
Madeni ambayo uongozi mpya ulipoingia
madarakani uliyakuta ni makubwa na yamelielemea shirikisho. Juhudi za kuongea
na wanaotudai ili aidha watupunguzie madai yao au tuyalipe kwa masharti nafuu
yanaendelea.Wale wote wanaotudai ambao wametuelewa katika hili tunawashukuru
sana. Kwa sasa kesi zote za madai dhidi ya TFF zilizokuwa mahakamani
zimeondolewa baada ya mapatano.
1. 4. Nidhamu
Nidhamu bado ni tatizo si kwa
wachezaji bali hata kwa viongozi wetu.Yupo mchezaji amediriki kupigana na
walinzi wa raia na wengine wakadiriki kumpiga mwamuzi,hili halikubaliki na
hatua kali zitakuwa zinatolewa dhidi ya watovu wa nidhamu bila kujali wao ni
kina nani kwenye mpira wa nchi hii.
1. 5. Maadili
Wizi mdogo mdogo hasa wa mapato ya
milangoni umeendelea.TFF tumekuta kesi za wizi wa aina hii zaidi ya hamsini
zilizoripotiwa polisi Chang’ombe na watuhumiwa hawakuwahi kupelekwa mahakamani
kwa kuwa mlalamikaji (TFF) hakujitokeza kuandika taarifa (statement). Uongozi
wangu umeamua utakuwa unafuatilia kwa karibu kesi hizi ili kukomesha tabia
iliyozoeleka ya udokozi.Pesa ya mpira itumike kwenye mpira.
1. 6. Maamuzi uwanjani (Refeering)
Wapo waamuzi wanaokosea kwa makosa ya
kibanadamu, hao tunawaelewa.Lakini zinapotokea tetesi au tuhuma za haki
kutotendeka kiwanjani kwa sababu nyingine zaidi ya hii shirikisho linashtuka
sana na kamwe halitakubali lidhalilike kwa tuhuma kama hizi.Shirikisho kwa sasa
linafuatilia kwa karibu kinachoendelea uwanjani ili kuhakikisha haki inatendeka
kwa timu zote.
Tayari mitihani imekwisha fanyika kupandisha madaraja waamuzi
mbali mbali ili kuongeza uwigo wa kupata waamuzi.Kozi za waamuzi zitaendelea
kutolewa ili kuzidi kunoa uwezo wao.
Aidha vituo vya kuendeleza waamuzi
vijana vya kambi ya Jenerali Twalipo na Alliance academy Mwanza viko mbioni
kuimarishwa ili viwe na nguvu zaidi ya kufundisha waamuzi vijana.
HITIMISHO
Ndugu zangu nihitimishe kwa kutoa wito
kwa wadau wote wa Mpira wa Miguu Tanzania wakiongozwa na Serikali, CAF,
FIFA, CECAFA, vyombo vya habari, Mashirika ya Umma, Mashirika yasiyo ya
Kiserikali, Makampuni na watu binafsi wote kwa pamoja tushikamane kwa pamoja
tukiwa na nia moja tu, kuinua kiwango cha mpira Tanzania na kuzifanya timu zetu
za mpira ziwe za wakubwa, za wanawake na za vijana ziwike, sio tu
barani Afrika, bali duniani pote. Kwa pamoja tunaweza.
Tukijaliwa tutakutana tena ndani ya
chumba hiki hiki baada ya siku 365 tangia nimechaguliwa kuongoza TFF ili
tufanye tathmini ya mwaka mmoja wa uongozi wangu. Mungu ibariki TFF
Mungu Ibariki Tanzania
Mungu ibariki Afrika
Jamal Malinzi
Rais wa TFF
07 Januari, 2014
No comments:
Post a Comment