Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi Bi. Hajjat Amina Mrisho Said (katikati) akizungumza na Wadadisi wa Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi wa mwaka 2014 kwa Kanda ya kasikazini inayojumuisha mikoa ya Tanga, Arusha, Kilimanjaro na Manyara. Kulia kwake ni Opio Mamu Msimamizi wa mafunzo katika kanda hiyo na kushoto kwake ni Juma Shaban Meneja Takwimu, Ofisi ya Taifa ya Takwimu mkoa wa Manyara. |
Wadadisi wa Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi wa mwaka 2014 kwa Kanda ya kasikazini inayojumuisha mikoa ya Tanga, Arusha, Kilimanjaro na Manyara wakimsikiliza kwa makini Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi Bi. Hajjat Amina Mrisho Said (hayupo pichani) katika mafunzo ya utafiti huo yanayotarajia kumalizika kesho jijini Tanga. |
Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi Bi. Hajjat Amina Mrisho Said (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wadadisi wa Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi wa mwaka 2014 kwa Kanda ya kasikazini inayojumuisha mikoa ya Tanga, Arusha, Kilimanjaro na Manyara. Mafunzo ya utafiti huo yanayotarajia kumalizika kesho jijini Tanga. |
.....................................................................................
(Picha zote na Veronica Kazimoto –
Tanga)
Na.Veronica Kazimoto na Aron Msigwa – Tanga.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu imewataka wadau mbalimbali
wakiwemo viongozi wa Serikali, siasa na waandishi wa habari kutumia takwimu
sahihi zinazotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu pindi wanapotekeleza majukumu
yao.
Akizungumza na waaandishi wa habari pamoja na
wadadisi wa Madodoso ya utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi mwaka
2014 kutoka kanda ya kaskazini leo jijini Tanga Kamishna wa Sensa ya Watu na
Makazi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bi. Hajjat Amina Mrisho Said amesema
kuwa ni jukumu la kila mtendaji katika eneo lake kuhakikisha kuwa
anatumia takwimu sahihi zinazotolewa na Ofisi hiyo.
Amesema Ofisi ya Taifa ya Takwimu ndiyo yenye
mamlaka na dhamana ya utoaji wa takwimu za masuala mbalimbali nchini na
kuongeza kuwa matumizi ya takwimu zisizo sahihi yana athari kwa jamii hasa
wakati wa kupanga mipango ya maendeleo kuanzia ngazi ya vijiji mpaka taifa.
Amesema kuwa takwimu sahihi huwezesha utekelezaji wa
mipango ya maendeleo na kuongeza kuwa zipo changamoto mbalimbali ambazo
ufumbuzi wake unaweza kupatikana kwa kufanya rejea ya takwimu sahihi kutoka
Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
“Takwimu ni muhimu sana katika kupanga namna ya
kukabiliana na matatizo na majanga mbalimbali yanayotokea katika jamii kama
mafuriko, njaa, masuala ya ardhi na elimu ambayo kimsingi yanahitaji matumizi
ya takwimu sahihi ili kujua kiwango halisi cha ukubwa wa tatizo na namna
ya kupata suluhisho la kudumu kwa wananchi husika.
Amesema ni vema wadau wanaotumia takwimu kwenye
majukwaa mbalimbali na waandishi wa habari kujenga tabia ya kuwasiliana na
Ofisi ya Taifa ya Takwimu kabla ya kutoa takwimu walizonazo ili kupata ukweli
wa hali halisi.
“Natoa wito kwa wadau mbalimbali na waandishi wa
habari kuhakikisha kuwa mnapata takwimu sahihi hata kama mmezipata kutoka kwa
viongozi, tafadhali hakikisheni mnapitia mamlaka husika kupata ukweli wa
takwimu hizo ili kuepuka kutoa takwimu zisizo sahihi”, Amesisitiza Kamishna wa
Sensa.
Ametoa wito kwa wadau mbalimbali kutembelea tovuti
ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu ikiwa ni moja ya chanzo sahihi cha habari katika
masuala yote yahusuyo takwimu na rejea sahihi na kuongeza kuwa takwimu zote
zinazotumika kutengeneza sera za taifa za mipango ya maendeleo zinatoka katika
chanzo kimoja tu ambacho ni Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
Katika hatua nyingine Kamishna wa Sensa ya Watu na
Makazi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bi. Hajjat Amina Mrisho Said ametoa wito
kwa Maofisa wa Takwimu walio katika mikoa na wilaya mbalimbali nchini kutumia
vikao mbalimbali vinavyofanyika katika Halmashauri na mikoa kutoa elimu ya
matumizi ya takwimu zilizopo ili waweze kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo
na kutatua kero mbalimbali za wananchi.
Amesema takwimu zilizopo lazima zitafsiriwe na
jukumu hilo lazima lifanywe na wawakilishi hao wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu
walio katika mikoa mbalimbali nchini na kuongeza kuwa wataalam hao kwa
kushirikiana na viongozi wengine wa halmashauri wana jukumu la kutoa elimu kwa
makundi mbalimbali ya jamii hasa vijana ili waweze kujiajiri na kutumia fursa
zilizopo katika maeneo yao ili kupunguza utegemezi.
“Naomba mtumie vikao hivyo vya hamashauri kutoa
elimu kwa sababu tayari ninyi mnazo takwimu, vikao vya halmashauri huwa
vinahusisha viongozi mbalimbali wa Serikali na jamii hivyo mnaweza kabisa
kushauri na kushawishi kwa viongozi hao kutumia takwimu sahihi ili kuondoa
matatizo mbalimbali likiwemo tatizo la ajira kwa vijana na kuondoa utegemezi
kwa kuwajengengea uwezo vijana wasio na ajira kujiajiri wenyewe”, amesema
Kamishna.
Aidha ametoa wito kwa watafiti na wadadisi wa
Madodoso ya Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi 2014 watakaoendesha zoezi la
utafiti wa idadi ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi kutoa elimu kwa vijana
ambao hawana kazi katika maeneo yote watakayopita ili kuwajengea uwezo wa
kufanya kazi pia kuwashauri kujiunga na vyuo vya ufundi Stadi (VETA) vilivyopo
katika maeneo mbalimbali nchini ili waweze kujiajiri na kuondoa wimbi la
utegemezi.
No comments:
Post a Comment