HAPA AKIKABIDHIWA WIZARA NA MH SHAMSI VUAI NAHODHA |
HAPA AKISALIMIANA NA BAADHI YA WATENDAJI WA WIZARA |
Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na JKT Bw. Job Masima
leo amewaongoza wakuu wa Idara, Vitengo na Taasisi za wizara hiyo kumpokea
Waziri wa Ulinzi Dkt Hussein Mwinyi (Mb) ambaye ameripoti wizarani hapo rasmi
baada ya kuteuliwa na Mhe. Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete kushika wadhifa huo
hivi karibuni.
Akimkabidhi wizara hiyo, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi
na JKT Mhe. Shamshi Vuai Nahodha amemuasa Waziri Mwinyi kuwa pamoja na majukumu
yake ni vema akatenga muda wa kutembelea miradi ya wizara hiyo, ikiwemo ujenzi
wa nyumba ili kuona mambo yanavyokwenda na kurekebisha dosari kabla miradi
haijafika mbali.
Kwa upande wake, Waziri Mwinyi amewataka viongozi wa
Wizara hiyo kufanya kazi kwa kasi kubwa kwani kipindi kilichobaki ni kifupi
sana kuelekea kwenye Uchaguzi mkuu ujao.
“Mwaka uliobaki wa kufanya kazi ni mmoja tu kwani
mwaka 2015 utakuwa na mambo mengi yanayohusiana na uchaguzi hivyo tulenge
kufanya kazi kubwa kufikia malengo yetu ndani ya mwaka huu mmoja kwa kasi
kubwa”, alisisitiza Mhe. Mwinyi.
Aidha, Mhe. Mwinyi alimshukuru Mhe. Nahodha kwa
mambo muhimu aliyoshauri ikiwepo kukamilisha yale yote aliyokuwa ameyaanzisha
kwa maslahi ya Wizara na Taasisi zake. Alimtakia kila la heri katika
majukumu yake ya uwakilishi na ubunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kabla ya makabidhiano hayo Wafanyakazi wa Wizara ya
Ulinzi walijipanga kwa safu ndefu kumpokea Waziri wa Ulinzi na JKT wakiongozwa
na viongozi mbali mbali waliohudhuria makabidhiano hayo wakiwemo Naibu Katibu
Mkuu Bibi Mwitango Rose Shelukindo, Mnadhimu Mkuu wa Jeshi Luteni Jenerali
Samuel Ndomba (aliyemuwakilisha Mkuu wa Majeshi), Mkuu wa Jeshi la Kujenga
Taifa Meja Jenerali Raphael Muhuga, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mzinga Meja
Jenerali Charles Muzanila na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Wizara ya Ulinzi na
JKT.
Hii ni mara ya tatu kwa Mhe. Mwinyi kuteuliwa
kuongoza Wizara hiyo. Kwa mara ya kwanza aliteuliwa mwaka 2008 hadi bunge
lilipovunjwa wakati wa uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Aidha, aliteuwa tena katika
Baraza jipya mwaka 2010 hadi 2012 alipohamishiwa Wizara ya Afya.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Ulinzi na JKT
No comments:
Post a Comment