MWAKA
1848, Mmishenari wa Kijerumani Dk Johan Ludwig Krapf, alitembelea
kijiji cha Magila kilichopo Muheza mkoani Tanga akiwa katika safari zake
za Afrika Mashariki.
Magila
kuna mlima ulio katika safu za milima ya Usambara ukipakana na mlima wa
Magoroto ambao ndio chanzo cha maji ya mto Mkurumuzi unaoelekea Muheza.
Historia
inaonyesha eneo la mlima Magila wenye miamba na mawe
mengi, zamani kabla ya kuja wageni lilitumika kuwatenga wagonjwa wa ukoma
na magonjwa mengine yasiyotibika, kwa lengo la kuwazuia wasiwaambukize wengine.
Dk
Krapf alipofika na kuwaona wagonjwa hao waliokuwa wakiishi kwa madhila
makubwa, alichonga msalaba katika mti wa mkuyu kwa imani kuwa Mwenyezi Mungu
angewaponya wagonjwa hao.
Eneo
hilo ndilo lililokuja kujengwa shule ya kwanza na Waingereza mwaka 1886. Alama
ya msalaba huo ipo hadi na sasa na ndipo ilipo Shule ya Sekondari
Hegongo.
Hadi
leo mahali hapo panaitwa Magila Msalabani. Kwa sasa Magila ni kata yenye vijiji
vya vya Magila, Mikwamba, Misongeni na Mafleta.
Mwandishi
wa Historia hii alifika katika eneo hilo nilipokuwa wilayani Muheza hivi
karibuni ili kuchunguza historia ya eneo hilo.
Hapo
nikutana na Luteni Kanali mstaafu John Mhina ambaye amekamilisha kuandika
kitabu kuhusu historia ya Magila Msalabani, kinachoeleza historia ya
kijiji hicho na ujio wa wazungu walioanzisha shule ya kwanza Tanganyika na
kanisa.
Luteni
Kanali Mhina aliyelitumikia Taifa kwa muda mrefu kama mwanajeshi , na baadaye
kuwa Mbunge wa Muheza kutoka mwaka 1990 hadi 1995, anasema harakati za
kuanzisha shule katika kijiji hicho zilitokana na Wamishenari waliokuja Afrika
Mashariki kutoka Ulaya kwaajili ya kueneza dini ya kikristo tangu miaka ya
1770.
Anawataja
baadhi ya Wamishenari hao kuwa ni pamoja na David Livingstone, Charles
Mackenzie, William Tozer na Edward Steer.
Anasema
harakati hizo zilianzia tangu visiwa vya Zanzibar mwaka 1863 ambako pia
walikomesha biashara ya utumwa na kuanza ujenzi wa kanisa la Anglikana la
Mkunazini Zanzibar kwa miaka 10 tangu mwaka 1873.
Anasema
wakati huo kulikuwa na shule iliyoanzishwa Zanzibar maeneo ya Kiungani na
Kiinua mguu na Askofu William Tozer mwaka 1869. Hata hivyo, anasema shule
hiyo haikuwa rasmi na ilikuwa ikifundisha elimu ya dini kwa watumwa
waliokombolewa.
Uamuzi wa kujenga shule Bara
“Mnamo
Agosti 13, 1967 Askofu Tozer alimtuma Padri CA Alington aende Vuga (Lushoto)
kwa Chifu Kimweri ili apate kibali cha kujenga kituo cha misheni kwenye maeneo
ya Bara,’’anasimulia Luteni Kanali Mhina na kuongeza:
“ Padri
Alington alimchukua Vincent Mkono aliyekuwa mwanafunzi wake wa Kiungani na
mwingine Mwinyi Khatib aliyekuwa mkalimali. Msafara huo ulipata baraka za
Sultan Majid aliyekuwa akitawala Zanzibar.”
Anaeleza
kuwa baada ya msafara wao kufika Vuga, Chifu Kimweri aliwasikiliza,
lakini akaomba apewe muda wa kutafakari kwanza.
Baadaye
Januari 20, 1868, Padri Alington alirudi Vuga na kuruhusiwa na
Chifu Kimweri kujenga sehemu yoyote katika maeneo ya Pwani.
Anasema
Padri Alington aliamua kuchagua eneo la Magila ambalo lilikwishajulikana
kutokana na alama ya msalaba uliowekwa na Dk Krapf.
“
Jumbe Kifungiwe aliyekuwa akiongoza Magila wakati huo chini ya baraza la
‘wamaka’ (Baraza la Wazee wa Kibondei), walimpa mlima wote wa Magila wakidhani
kuwa atashindwa kujenga kwa sababu ya kuwa na mawe mengi….kwa mshangao
aliporudi aliyatumia mawe hayo kujengea.” anaeleza.
Anasema
pamoja na kazi ya kueneza dini Wamishenari hao walijipa jukumu la kuwatunza
wagonjwa wa ukoma na kuanzisha shule.
“Shule
ya sokoni ilikuwa kwanza kujengwa maeneo hayo mwezi Aprili 1869 chini ya Padri
Fraser na wanafunzi wake walikuwa ni pamoja na Jumbe Kifungiwe na ndugu yake
Sagosago na vijana wengine. Palikuwa na soko dogo na mti mkubwa wa
Mzindanguuwe, watu wazima walipenda kukaa hapo ili walione jambo hilo geni,”
anaongeza kusema.
Sekondari ya Hegongo
Hivi
sasa eneo hilo kuna shule iitwayo Hegongo. Mkuu wa shule hiyo, Wilfred Mdimu anasisitiza kuwa
eneo hilo ndipo palipojengwa shule ya kwanza Tanzania ambapo mpaka
sasa kuna mabaki ya darasa la kwanza lililojengwa na Wamisheni.
Hivi
sasa anasema darasa hilo linatumiwa kama ofisi ya walimu wa shule ya sekondari
ya kata Magila.
“Hili
ndilo darasa la kwanza lililojengwa mwaka 1869 na Waingereza. Awali lilikuwa
ghorofa lakini likabadilishwa. Inasemekana shule nyingine ilijengwa Bagamoyo na
baadaye Minaki,” anasema Mdimu na kuongeza,
“Walijenga
pia kanisa baada ya lile la Mkunazini Zanzibar. Lakini lilipochakaa ndipo
wakajenga kanisa jingine mwaka 1886 kama lile la Mkunazini na ndiyo linatumika
hadi sasa.”
Akizungumzia
uchaguzi wa eneo hilo, Mdimu anasema awali wazungu walitaka kujenga shule
maeneo ya Muhenza Mkumbi na Mkanyageni, lakini wakaathiriwa na malaria,
ndipo wakahamia katika mlima wa Magila.
Kuhusu
shule hiyo, Mdimu anasema kuwa awali ililenga kuwaandaa Waafrika ili wawasaidie
wamisheni katika kazi zao. Waliwafundisha kusoma, kuandika na kuhesabu.
Baadaye
elimu ikapanuka baada ya shule za St. Marys na St Martin kujengwa zikiongeza
masomo na wanafunzi.
Anaongeza
kuwa shule hizo hazikudumu muda mrefu, bali zilibadilishwa na kuwa Sekondari ya
wasichana ambayo nayo ilikuja kuhamishiwa wilayani Korogwe ilipo shule ya
wasichana maarufu kwa jina la Korogwe girls.
Baada
ya kuhamisha shule hiyo, matumizi yakabadilishwa na kikaanzisha chuo cha
ualimu kwa wanawake tu. Hata hivyo, anasema chuo hicho nacho
kilihamishiwa tena Korogwe kilipo chuo cha ualimu hadi leo.
“
Mwaka 1974 hadi 75, majengo hayo yakafanywa kuwa mahali pa kujifungulia
wanawake na ndipo ilipoanzia hospitali teule ya Muheza. Lakini ikahamishiwa
eneo ilipo sasa na majengo haya yakabaki matupu,” anasema Mdimu.
Kuanzishwa kwa Hegongo sekondari
Mwalimu
Mdimu anasema baada ya majengo kubaki matupu, mwaka 1976 wenyeji wa Magila
walimwomba Askofu wa kanisa hilo dayosisi ya kaskazini John Ramadhani,
ili waanzishe shule ya sekondari hasa kwenye majengo ulipo msalaba wa Dk Krapf,
naye akawakubalia.
“Februari
24, 1977 shule ya Hegongo ilianzishwa ikiwa chini ya wenyeji wa Magila ili
kuwapa elimu watoto wa wilaya hiyo,” anasema.
Hata hivyo
anasema shule hiyo haikuwa na maendeleo mazuri kwa muda mrefu. Isitoshe,
wasimamizi wa shule hiyo walishindwa kuiendesha kutokana na madeni makubwa ya
umeme, mishahara ya watumishi na mafao yao.
Hegongo ya sasa
Anasema
hadi mwaka 2000 wasimamizi wa shule hii walishindwa kabisa kuiendesha
wakairudisha kwa kanisa.
“Tangu
wakati huo uongozi wa kanisa umeamua kuiendesha kwa kwa kulipa madeni makubwa
yaliyokuwepo na kuimarisha hali ya elimu,” anasema na kuongeza:
“Kwa
sasa tunaboresha majengo, tumejenga maabara, maktaba ya kisasa na
tutaongeza nyingine. Askofu wa sasa ameamua kuwachukua mapadri 10 waliomaliza
kidato cha sita na kuwapeleka vyuo vikuu ili wasomee ualimu kwa ajili ya shule
hii.’’
Kwa
upande mwingine, majengo ya zilizokuwa shule za St. Mary’s na St.
Martin sasa zimechukuliwa na Serikali, huku mojawapo ikitumika kama shule
ya sekondari ya kata ya Magila na nyingine kama shule ya msingi.
Source;Mwananchi
No comments:
Post a Comment