Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Costantine Masawe |
Watu watano wa familia moja wamefariki dunia na wengine wawili kunusurika baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupata ajali mkoani Tanga.
Ajali hiyo ilitokea juzi saa 6:30
mchana katika kitongoji cha Mtakuja, kata ya Misima, wilayani Handeni, kwenye
barabara kuu ya kutoka Handeni kuelekea Korogwe.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Tanga, Costantine Masawe, gari lililopata ajali hiyo lilikuwa na watu saba wa
familia moja, huku wawili wakinusurika katika ajali hiyo.
Kamanda Masawe aliwataja watu waliyokufa kwenye ajali hiyo kuwa ni, Athumani Yussuph (45), Zahara Chayungo (35), Mwajuma Mzimo (55), Juma Hossein (90) na Zuber Abdulrahman (35) na kwamba majeruhi mmoja ndiye aliyetambuliwa huku mwingine ikisadikiwa aliondoka eneo hilo baada ya ajali.
Akielezea mazingira ya ajali hiyo,
Kamanda Masawe alisema ilihusisha gari aina ya Noah yenye namba za usajili T
493 AUH.
Alieleza kuwa gari hilo lililokuwa likiendeshwa na Miraji Shaban (22) ambaye ni majeruhi ilipofika eneo hilo ilikatika shafti hali iliyosababisha kupoteza muelekeo na kupinduka.
Alieleza kuwa gari hilo lililokuwa likiendeshwa na Miraji Shaban (22) ambaye ni majeruhi ilipofika eneo hilo ilikatika shafti hali iliyosababisha kupoteza muelekeo na kupinduka.
Kamanda Massawe alisema kuwa gari hilo lilikuwa limebeba watu saba wa familia
moja na kwamba mmoja wa watu wanaosadikiwa kuwa ni majeruhi ambaye hakufahamika
jina alitoweka muda mfupi baada ya kutokea kwa ajali hiyo.
Miili ya marehemu hao ilipelekwa katika
Hospitali ya Wilaya ya Handeni na kuchukuliwa baadaye na ndugu na jamaa kwa
ajili ya mazishi katika kijiji cha Misima.
Kamanda Masawe alitoa wito kwa madereva
kuwa makini wakati wote wawapo barabarani, kwenda mwendo wa kawaida pamoja na
kuvifanyia uchunguzi wa mara kwa mara vyombo vya usafiri kabla ya kuanza
kuvitumia ili kuepuka majanga kama hayo.
Aidha, aliwataka wasafiri na hata wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa pale wanapomuona dereva akifanya ukiukwaji wa sheria za barabarani kama vile mwendo kasi, ulevi na kujishughulisha na kitu kingine anapoendesha kama matumizi ya simu za mkononi.
Alisema jamii inategemewa na jeshi hilo
katika kufanikisha harakati za kukabiliana na matendo ya uovu zikiwamo ajali za
barabarani ambazo huleta ulemavu na kupoteza maisha ya watu kwa kiwango
kikubwa.
No comments:
Post a Comment