TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imevitoa
wasiwasi vyama vya siasa kuwa hakutakuwepo na wizi na udanganyifu wa kura
katika matokeo ya uchagauzi wa rais, wabunge na madiwani, utakaofanyika nchini
kote Oktoba 25, mwaka huu.
Aidha, NEC
imesema ipo tayari kushirikiana na wataalamu wa vyama hivyo kubaini vyanzo vya
wizi wa kura, iwapo tatizo hilo litajitokeza na hivyo kuhakikisha haki
inatendeka kwa vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi huo.
Hayo
yalisemwa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji mstaafu Damian
Lubuva wakati wa mkutano wake na wawakilishi wa vyama vya watu wenye ulemavu,
aliokutana nao kupata ushauri na maoni ya taasisi hizo kuelekea uchaguzi mkuu
wa Oktoba mwaka huu.
Alisema
hadi kufikia sasa, vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi huo vimefanyika kampeni
za kistaarabu. Lakini, alisema katika siku za hivi karibuni, baadhi ya vyama
vimekuwa vikitoa kauli na matamshi yaliyovuka mipaka. Alisema NEC inavionya
vyama hivyo kuacha mara moja tabia hiyo.
“Vipo baadhi ya vyama vya siasa
na wagombea wao wamekuwa wakitumia muda mwingi kutoa lugha zisizofaa baada ya
kunadi sera ya vyama vyao, vyama hivyo tumekutana navyo na kuwataka kuacha mara
moja kampeni za aina hiyo,” alisema Jaji Lubuva.
Jaji Lubuva
alisema Julai 27 mwaka huu, vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi mkuu,
vilisaini mkataba wa maadili ya uchaguzi huo, hivyo ni wajibu wa vyama hivyo
kuzingatia viapo walivyotoa katika maktaba huo.
Akifafanua,
Jaji Lubuva alisema iwapo chama chochote hakina hoja ya kuzungumza na wananchi
ni vyema kikawa kimya hadi siku ya uchaguzi Oktoba 25 mwaka huu. Aidha, Jaji
Lubuva alivitaka vyama vya siasa kuacha tabia ya kuingilia masuala ya utawala
ya tume hiyo, kwani kufanya hivyo vyama hivyo vitakuwa vikifanya kazi za tume
hiyo na hivyo kuingilia masuala ya ndani ya kiutendaji ya taasisi hiyo.
Akizungumzia
maandalizi ya uchaguzi huo, Jaji Lubuva alisema mahitaji yote ya msingi ya
uchaguzi huo tayari yamepokewa na NEC, ikiwemo karatasi, wino, na masanduku ya
kura, ambapo baadhi yake yameanza kusafirishwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Akisisitiza
juu ya kuamini utendaji wa tume, alisema haioni sababu ya vyama hivyo kuwa na
wasiwasi na tume na kutaka kubaki vituoni kwa madai ya kulinda kura. Alisema
matokeo ya uchaguzi mkuu, yatatangazwa kwa mujibu wa sheria na taratibu na
mapema iwezekanavyo, tofauti na siku saba sheria inavyotaka, huku kukiwa na
waangalizi 140 kutoka Umoja wa Ulaya (EU) na wengine wa nje.
Waangalizi
wa ndani watakuwa 75. Wapigakura wanatakiwa kurejea nyumbani mara tu baada ya
kupiga kura na hawatakiwi kuendelea kukaa vituoni kwa madai kulinda kura.
Aidha, alisema Tume imepokea taarifa ya vifo vya wagombea watano wa nafasi za
udiwani na vifo vya wagombea wawili wa nafasi ya ubunge, ambapo uchaguzi katika
maeneo hayo umeahirisha hadi Novemba 22 mwaka huu.
Alisema
katika uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka huu, NEC imefanya uteuzi wa wagombea nane wa
urais, wagombea 1,218 wa ubunge, kati yao wanaume wakiwa 985 na wanawake 233.
Kwa upande wa udiwani ni 10,879, kati yao wanaume ni 10,191 na wanawake 679.
Akizungumzia
walemavu wasioona, alisema watatumia kifaa maalumu cha ‘Tactile Ballot
Folder’kupigakura, ambacho kitamwezesha mlemavu huyo kupiga kura yake mwenyewe
bila kusaidiwa na mtu mwingine, hivyo kutimiza lengo la usiri wa kura kwa
mpigakura.
Kuhusu daftari
la kudumu la wapiga kura, Jaji Lubuva alisema katika kipindi cha siku 10 zijazo
kuanzia sasa, Tume hiyo inatarajia kusambaza daftari la kudumu katika mikoa
yote nchini na wananchi watatakiwa kuhakiki majina yao katika kipindi cha siku
8.
CHANZO: HABARI LEO
No comments:
Post a Comment