Mkuu wa Mkoa Mh. Chiku Gallawa akizungumza na Maafisa Uwekezaji |
Maafisa Uwekezaji wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mh. Chiku Gallawa |
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mh. Chiku Gallawa amewataka maafisa uwekezaji viungo wa Halmashauri zote mkoani hapa kuwa wabunifu wa kuibua vivutio vitakavyowavutia wawekezaji na hatimaye waweze kubadilisha kipato cha Mwananchi wa Tanga na kufikia Tsh.1,500,000/- kwa mwaka.
Gallawa ameyasema hayo
juzi katika kikao kazi na maafisa hao kilicholenga kuwatambulisha maafisa
uwekezaji wa wilaya na kufanya tathmini ya maendeleo ya hali ya uwekezaji baada
ya kongamano lililofanyika Septemba 2013 likijumuisha mikoa ya kanda ya
kaskazini kwa lengo la kutangaza fursa ilizonazo.
Alisema kuwa kipaumbele
cha mkoa kufikia 2015 ni kuongeza pato la Mwananchi hivyo amewaita maafisa hao
ili waweze kueleza wamefanya nini mara baada ya kumalizika kwa kongamano la
Septemba na mikakati yao ya kuendeleza uwekezaji katika mkoa wa Tanga.
“Nimewaita hapa
ili mpate kufahamiana,kubadilishana
uzoefu na kuweza kushirikiana katika kukuza uwekezaji ndani ya mkoa na hatimae
muweze kuongeza kipato cha Mwanatanga kwani hicho ndiyo kipaumbele chetu
kufikia 2015.” Aliongeza Gallawa.
Aidha aliongeza kuwa
maafisa uwekezaji wanapaswa kuwa wabunifu,waaminifu na wenye uwezo wa kutambua
fursa zilizopo pamoja na taasisi wanazoweza kushirikiana nazo katika maswala ya
uwekezaji kama MUVI na SIDO waliokuwa washiriki wa kikao hicho na kueleza kuwa
Mkoa unajipanga kuwajengea uwezo wa kitaalamu maafisa hao ili waweze kutimiza
lengo.
Kwa upande wake afisa
uwekezaji wa mkoa Mussa Mlawilo aliwataka maafisa hao kuongeza ufanisi katika
kushughulika na mpango wa ubia wa sekta binafsi na sekta ya umma katika
uwekezaji (PPP) ili kujenga uchumi hai na endelevu wa mkoa.
Kadhalika aliongeza
kuwa maafisa hao wanapaswa kuwa wakarimu na wenye kujali zaidi huduma kwa mteja,
kuepukana na migogoro na hatimae kuvuta wawekezaji wapya kwani wawekezaji hao
wakichukua 75% ya fursa zilizopo mkoani Wananchi wa Tanga wataondoka katika
hali ya umasikini,kuongeza pato la taifa na maafisa hao watakuwa ni mfano wa
kuigwa kwa kuwajibika ipasavyo .
No comments:
Post a Comment